Kwa mujibu wa Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanchi, Imamu wa Ijumaa wa Najaf Ashraf, katika hotuba ya Swala ya Ijumaa aliyotoa katika Husseiniya Kuu ya Fatimiyya, iliyopo Najaf Ashraf, alizungumzia masuala mbalimbali ya ndani ya nchi, kikanda na kimataifa.
Serikali Inapaswa Kulaani Mashambulizi ya Mabomu Dhidi ya Watu wa Yemen Kabla ya Kuitetea Saudi Arabia
Akizungumzia masuala ya kikanda, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanchi alieleza kuwa; serikali ya Iraq imelaani mashambulizi ya Wahuthi (Ansarullah ya Yemen) dhidi ya viwanja vya ndege vya Saudi Arabia. Hata hivyo, alisisitiza: “Haturidhii wala hatukubali Waislamu kupigana wao kwa wao. Lakini ni muhimu kwanza kulaani mashambulizi ya mara kwa mara ya mabomu dhidi ya Wahuthi, pamoja na muungano ambao Saudi Arabia imeuita ili kuwakandamiza Wahuthi, chini ya uongozi wa Marekani na kwa ushiriki wa Israel, Pakistan na Uturuki.”
Aliongeza: “Anayeanzisha dhuluma ndiye dhalimu zaidi. Inashangaza kuona ukimya kuhusu mashambulizi dhidi ya Wahuthi, huku kukiwa na haraka ya kulaani mashambulizi dhidi ya viwanja vya ndege vya Riyadh na Dammam.”
Kulaani Mashambulizi ya Mabomu Ghaza, Lebanon na Syria, Huku Nchi za Kiarabu Zikiwa Kimya
Imamu wa Ijumaa wa Najaf Ashraf alisisitiza kwamba; ni wajibu wetu kwanza kulaani mashambulizi ya mabomu yanayoendelea dhidi ya Ghaza na wakazi wake, mashambulizi yanayoendelea kusini mwa Lebanon, pamoja na mashambulizi yanayoendelea nchini Syria.
Alibainisha kuwa; Benjamin Netanyahu alisema jana kwamba Israel haitajiondoa katika maeneo ambayo imeyakalia hivi karibuni nchini Syria na Lebanon. Alisema kuwa yote haya yanaendelea huku nchi za Kiarabu zikiwa kimya, bila kutoa hata tamko lolote la kulaani matukio hayo.
Kupiga Marufuku Hijabu Nchini Azerbaijan ni Kuingilia na Kukashifu Maadili ya Kiislamu
Akizungumzia masuala ya kimataifa, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadruddin Qabanchi alilaani marufuku ya kuvaa hijabu kwa wanafunzi na walimu katika shule za Azerbaijan.
Alisema kuwa, licha ya Waislamu kuunda asilimia 95 ya wakazi wa Azerbaijan, serikali ilichukua uamuzi huo na kuanza kuutekeleza, jambo lililosababisha kufukuzwa mamia ya maelfu ya wanafunzi kutoka shuleni, pamoja na walimu.
Alihoji: “Haki za wanawake ziko wapi? Uhuru wa mtu binafsi uko wapi? Demokrasia wanayojivunia iko wapi? Demokrasia imegeuzwa kuwa kauli mbiu ya uongo inayotumiwa kupambana na dini. Mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu yako wapi?”
Imamu wa Ijumaa wa Najaf Ashraf aliitaka serikali ya Iraq ilaani hatua hiyo na kutangaza mshikamano wake na wananchi na familia za Azerbaijan, wanaume kwa wanawake.
Alisisitiza kwamba suala hili si jambo linalohusu eneo fulani au kabila fulani pekee, bali ni uvamizi dhidi ya maadili yetu ya Kiislamu. Alimalizia kwa kusisitiza kwamba: “Yeyote asiyejali mambo yanayowahusu Waislamu, basi si miongoni mwao.”
Maoni yako